HOJA tatu za msingi zinatarajiwa kutumiwa na Jopo la Majaji
watatu wa Mahakama ya Rufani, kuamua rufaa ya kesi ya aliyekuwa mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema katika hukumu inayotarajiwa kusomwa leo
jijini Dar es Salaam.
Kati ya hoja 18 zilizowasilishwa na upande wa
rufaa kupinga hukumu hiyo, zipo hoja tatu ambazo zinaonekana za msingi
katika hukumu ya leo itakayotolewa na majaji waliokuwa wakisikiliza kesi
hiyo; Salum Massati, Bernard Luanda na kiongozi wao, Nathalia Kimaro.
Lema
alivuliwa ubunge Aprili 5, 2012 katika hukumu iliyotolewa na Jaji
Gabriel Rwakibalira, kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa
CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kutokana na hukumu hiyo, Lema, kupitia kwa
Wakili wake, Method Kimomogoro alikata rufaa Mahakama ya Rufani,
akiwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu hiyo.
Hoja ya kwanza ni kama mpigakura anaweza
kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi kwa niaba ya
mgombea husika aliyeshindwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Wakili
Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis alidai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha ilikosea kutengua ubunge wa Lema, kutokana na kesi iliyofunguliwa
na walalamikaji wanaodai kuwa ni wapigakura.
Wakili Vitalis, aliyemwakilisha Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), ambaye pia alikuwa upande wa Lema, alidai kuwa
wajibu rufaa hawakuwa na haki ya kufungua kesi kupinga ushindi wa
mrufani (Lema) kwa kasoro zilizotokea wakati wa kampeni.
Vitalis alidai kuwa, wajibu rufani hao
hawakuwa wahusika katika mchakato huo wa kampeni na hivyo hawakuwa na
haki ya kupinga matokeo hayo mahakamani.
Akifafanua zaidi, Wakili Vitalis alidai kuwa
anayepaswa kufungua kesi mahakamani kwa madai ya lugha ya matusi ni yule
aliyetukanwa kwa kuwa hayo ni maumivu ya mtu binafsi na kwamba hata
anapokufa, madai yake nayo hufa wala hayawezi kuendelezwa na mtu
mwingine.
“Sasa iweje kwa mtu ambaye yuko hai, lakini watu wengine ndio waje mahakamani kufungua kesi? Alihoji Wakili Vitalis.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mawakili wa
mrufani, Method Kimomogoro na mwenzake ambaye pia ni Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Wakili Kimomogoro alidai kuwa, Jaji alikosea
kuamua kuwa mtu yeyote aliyejiandikisha kupiga kura ana haki isiyo na
mpaka ya kufungua kesi kupinga matokeo.
Alidai kuwa, hoja yao ni
kwamba mtu anakuwa na haki hiyo pale ambapo haki yake imevunjwa au
inaelekea kuvunjwa na si pale aliyeathirika na ukiukwaji wa haki hiyo ni
mtu mwingine.
Kwa upande wake, Lissu alidai kuwa mpigakura
ana haki ya kupinga matokeo mahakamani kwa madai kuwa haki zake pale
ambapo madai yao yanaambatana na haki zilizotajwa kwenye Katiba ambazo
ni pamoja na haki ya kupiga kura.
Majibu ya Warufaniwa
Akijibu hoja hiyo,
Wakili wa warufaniwa, Alute Mughway alidai kuwa haki hiyo inaelezwa
katika kifungu cha 111 (1) (A) cha Sheria ya Uchaguzi (2010) pamoja na
Katiba na sheria nyingine za nchi na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi
zinazokataza siasa za majitaka.
Uamuzi wa Mahakama kuhusu hoja hiyo
ndiyo ama utahitimisha hukumu hiyo bila kujadili na kuzitolea uamuzi
hoja nyingine, ikiwa mahakama itaamua kuanza na hoja hiyo, au
utakaoruhusu kuendelea na mjadala na kisha uamuzi wa hoja nyingine
kutolewa.
Ikiwa mahakama itakubaliana na hoja za warufani kuwa katika
mazingira ya kesi hiyo, mpigakura hakuwa na haki ya kufungua kesi
mahakamani kupinga matokeo hayo, basi hoja nyingine zitakuwa zimekufa na
Lema atarejea bungeni.
Hata hivyo, mahakama haiwezi kufumbwa midomo
kuendelea kujadili na kutoa uamuzi kwa hoja nyingine, ikiwa itaona ni
vyema kwa lengo la kuweka msingi mzuri na mwongozo katika uamuzi wa
mashauri mbalimbali yanayoweza kujitokea baadaye.
Ikiwa mahakama
itakubaliana na wajibu rufaa kuwa katika mazingira hayo mpigakura ana
haki kupinga mahakamani matokeo hayo, basi mahakama itabidi kuendelee na
hoja nyingine.
Hoja nyingine
Hoja nyingine ni matumizi ya
lugha za matusi katika kampeni, ambayo ni moja ya hoja za msingi
zilizomvua ubunge Lema, baada ya Jaji Rwakibarila kuthibitisha kwamba
alimtukana aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian.
Katika hoja hiyo, Wakili Vitalis alidai kwamba
hata kama kulikuwa na lugha ya matusi kama wajibu rufaa walivyodai
katika ushahidi wao mahakama haikustahili kumvua Lema ubunge kwa kuwa
Bunge liliruhusu matusi kwenye kampeni.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 108
cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 313 ya mwaka 2010, matusi si miongoni mwa
mambo ambayo yanaweza kutengua matokeo ya uchaguzi.
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa, Bunge
liliruhusu kutukanana baada ya kufanya marekebisho katika sheria ya
uchaguzi, mwaka 1995 kufuatia hukumu ya kesi kati ya AG dhidi ya Aman
Kabourou.
Alifafanua kuwa awali sheria ilikuwa inaruhusu
matokeo ya uchaguzi kutenguliwa kutokana na lugha za matusi, kama
ilivyotokea kwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Karatu, mwaka 1995.
“Baada
ya hukumu ya kesi ya Kabourou, Januari, 1995, mwezi Julai mwaka huo
Bunge lilifanya marekebisho na kuondoa suala la matusi katika mambo
yanayoweza kutengua uchaguzi,” alidai na kuongeza:
“Hapa Bunge liliifunga mikono mahakama, hakuna
kutengua matokeo ya uchaguzi kwa mambo ambayo hayajatajwa. Kwa uamuzi
huu waliamua kutukanana, kwa hiyo nasi hatuwezi kuwakatalia”.
Pia alidai kuwa, kifungu cha 108 (2) cha
Sheria ya Uchaguzi kinaeleza aina za ubaguzi zinazokatazwa ni pamoja na
kidini na kikabila na kwamba aina nyingine kama makazi (Uzanzibar,
Ubara) hazijatajwa.
Kuhusu hoja ya matumizi ya lugha ya matusi
katika kampeni, Wakili Mughway alipinga madai ya Wakili wa Serikali,
akidai kuwa si ya kweli na kwamba alikuwa akiipotosha Mahakama.
“Sikubaliani
na maneno ya AG (kupitia wakili wa Serikali Vitalis) kuwa ni ruksa
wanasiasa kutukanana,” alidai na kusisitiza kuwa madhumuni ya kukataza
vitendo hivyo ni kudumisha siasa safi na kuhakikisha nchi inatawaliwa na
siasa safi.
Mbali na hoja hizo, zingine zinazoweza
kutumika na majaji hao kutoa hukumu hiyo ni madai kuwa Jaji alitumia
ushahidi wa mdomo bila kuungwa mkono na ushahidi mwingine na kwamba
aliegemea ushahidi wa walalamikaji na mashahidi wao tu.