Na . Ramadhan Ali na Mwanaisha Mohammed-Maelezo
Askari mmoja wa Jeshi la Polisi
F.2105 Coplo Said Abdulrahaman wa Kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi ameuliwa
kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi kazini majira
ya saa 6.30 usiku katika eneo la Bububu.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake Ziwani, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa
amesema mauaji hayo yamesababishwa na fujo za wafuasi wa Jumuiya ya UAMSHO
baada ya kuenea uvumi wa kutekwa Msemaji Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi
usiku wa kuamkia jana.
Kamishna Mussa amesema Jeshi
la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watu waliofanya mauaji ya Coplo
Saidi Abdulrahaman ili kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani kama sheria za nchi
zinavyowaelekeza.
Amesema mpaka hivi sasa watu
10 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali yaliyotokana na vurugu za jana
na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa Sheikh Farid unaendelea.
Ameongeza kuwa kutekwa kwa
Sheikh Farid kunatia mashaka kutokana na mazingira ya kutoweka kwake kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake Said Omar Said ambae alikuwa dereva wake
katika hatua za mwisho maeneo ya Mazizini walipokwenda kununua umeme.
“Sheikh Farid alimuamuru Said
amuache katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka umeme na wakati huo akaendelea
na mazungumzo na watu wengine walikuwemo ndani ya gari nyengine ndogo ya NOAH
ambayo nambari zake hazijajulikana lakini aliporudi kumchukua hakumkuta”
alisema Kamishana Mussa.
Amesema fujo hizo
zilisababisha hasara kubwa kwa Serikali, Chama tawala na wananchi ikiwemo
kuchoma na kuharibumiundo mbinu ya barabara, kuharibu maskani za CCM za Kisonge
na Muembeladu kwa kuzichoma moto baadhi ya magari kuvunjwa vioo na kuvunja duka
la pombe na kuiba mali iliyokuwemo ndani.
Hata hivyo amedai hali ya Mji
wa Zanzibar kwa sasa ni shwari, wananchi wanaendelea na shughuli zao kama
kawaida na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vyengine vya ulinzi na
usalama vitaendelea kuhakikisha amani inadumu muda wote.
Amewataka wananchi kuendelea
kuwa wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao, na kutoa
taarifa za watu waliohusika na vurugu pamoja na mauaji ya Coplo Said
Abdulrahaman.
Mwisho IMETOLEWA NA MAELEZO
ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment
This is a public viewable website, post something that is not harmful to other people