LICHA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kunyakua viti 22 kati ya 29 vya
udiwani katika uchaguzi uliofanyika juzi, chama hicho tawala kimepoteza
kata nne kilichokuwa kinazishikilia kabla ya uchaguzi huo.
Uchaguzi huo ulifanyika kuziba nafasi zilizoachwa wazi na madiwani walioondoka kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo vifo.
Matokeo ya uchaguzi huo yanaonyesha kwamba katika Kata 29, Chadema wameshinda katika kata tano na kukifanya kuongeza madiwani watatu. TLP na CUF kila kimoja kimepata kata moja.
Kabla ya uchaguzi huo, Chadema kilikuwa na Kata mbili za Rombo na Mvomero ambazo kimefanikiwa kuzitetea na kuongeza nyingine tatu, ambazo ni Mlangila (Ludewa), Ipole (Tabora) na Daraja Mbili (Arusha) ambazo awali, zilikuwa zikishikiliwa na CCM.
TLP kilitetea kiti chake katika Kata ya Vunjo (Kilimanjaro) wakati CUF kilitwaa Kata ya Newala ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na CCM.
CCM kimetetea viti vyake vingine vilivyobaki ambavyo ni Msalato (Dodoma), Bang’ata (Arumeru Magharibi), Mletele (Songea), Mwawaza (Mjini Shinyanga), Lwezera (Geita), Bugarama (Kahama) na Bagamoyo mkoani Pwani.
Viti vingine ni Mnero na Miembeni (Nachingwea), Myovizi (Mbozi), Mpapa (Momba), Mahenge (Ulanga), Vugiri (Korogwe), Tamota (Lushoto), Makata (Liwale), Mpepai (Mbinga), Kiloleli (Sikonge), Miyenze (Tabora), Karitu (Nzega), Lubili (Misungwi), Kilema Kusini (Moshi), Nanjara/Neha (Rombo), Lokokona (Nanyumbu) na Kitangiri (Newala).
Katika Kata ya Rwezera, Misango Jeremiah alishinda baada ya kupata kura 1,309 dhidi ya wapinzani wake, Ibuga Mussa (Chadema) aliyepata kura 933 na Mussa Mtagala (CUC) aliyepata kura 317. Uchaguzi huo ulifanyika kujaza nafasi hiyo iliyokuwa wazi baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo, Anatory Mkufu kufariki dunia kwa ajali ya gari Februari 23, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
This is a public viewable website, post something that is not harmful to other people