MIGOGORO ya kidini, imeendelea kushika kasi baada ya watoto wawili
waumini wa dini ya Kiislamu, kudaiwa kuchoma moto vitabu 10 vya
uchambuzi wa Biblia ndani ya madhabahu ya Kanisa Katoliki la Msumi
lililopo Mbezi mjini Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea Novemba 22, mwaka huu saa 10 jioni, wakati
waimbaji wa kwaya wa kanisa hilo walipokuwa wakijiandaa kuingia kwa
ajili ya kufanya mazoezi.
Akizungumza na MTANZANIA, msimamizi wa
Kanisa hilo, Katekista Costantine Safi, alisema watoto hao wenye umri
kati ya miaka 11 hadi 13, walichoma vitabu hivyo wakati yeye akiwa
anafanya usafi nje ya kanisa.
“Hawa watoto walivizia nikiwa nje
ya kanisa, nikiwa nafanya usafi, wakati huo wanakwaya walikuwa
wanajiandaa kuingia kanisani kwa ajili ya kufanya mazoezi, hivyo
nilifungua milango ya kanisa ili waingie.
“Lakini ghafla watoto
hao, waliingia hadi kwenye altare (madhabahuni) na kukuta vitabu 10 vya
shajara ambavyo ni vipya na vililetwa na uongozi wa kanisa kwa ajili ya
kuwagawia waumini.
“Kama ilivyo kawaida mbele ya kanisa huwa
kunakuwa na viberiti kwa jili ya kuwashia mishumaa, kwa maana hiyo
walitumia viberiti hivyo kuchoma moto vitabu hivyo.
“Badaa ya
baadhi ya wanakwaya kuanza kukaribia kuingia ndani, watoto hao
walikimbilia barabarani na kujichanganya na makundi ya vijana waliokuwa
wakienda kucheza mpira, lakini kwa kuwa tayari walikuwa wameshabainika
na kuanza kukimbizwa na wanakwaya hao, tuliweza kuwakamata na kuwapeleka
katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Msumi.
“Hata hivyo, Ofisa
Mtendaji wa Mtaa huo, alitushauri kuwa suala hili tulipeleke polisi kwa
kuwa ni kubwa, tuliandikiwa barua ya maelezo, tukaiwasilisha kwa Paroko
wa Kanisa letu Father Anthony, ambaye alitushauri tuonane kwanza na
wazazi wa watoto hao ili tuwasamehe.
“Ndipo tukaenda kwa wazazi
wa watoto hao, ambapo mzazi wa kwanza ni Ismail Sadick na wa pili Ismail
Said, tuliwaeleza tukio hilo, lakini tukawaambia tumewasamehe watoto
hao ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Msumi, wakafurahi na kuunga
mkono hatua hiyo.
“Tuliona ni vyema tutoe taarifa kwenye uongozi
wa jimbo, ambapo tulienda kuonana na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar es
Salaam, Eusebius Nzigirwa, alitushauri tutoe taarifa polisi.
“Askofu
wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Policarp
Kadirnali Pengo ameshauri hivyo hivyo ili yasije yakazuka mengine
makubwa zaidi.
“Tulienda kuripoti na kupewa RB namba MKB/RB/918/2012 ya Novemba 23, mwaka huu,” alisema.
Baadhi
ya waumini, walidai kumekuwapo na kikundi cha waumini wa dini ya
Kiislamu, ambao wanadaiwa kutoa fedha kwa vijana wanaowatuma kuharibu
mali za makanisa ya Kikristo.
“Ingawa hapa kwetu hatuna uhasama
kabisa na hawa wenzetu, tumeshindwa kuelewa kwa nini wametufanyia hivi
kwa sababu kwanza vitabu hivi ni vipya na vimenunuliwa kwa gharama kubwa
ya zaidi Sh 200,000.
“Pia tumeshaanza kupatwa na wasiwasi, kwa
sababu tumesikia kuwa kuna kikundi cha Waislamu kinafadhili vijana,
wanaotumwa kuharibu mali za madhehebu yetu, inasemekana wanalipwa kati
ya Sh 100,000 na kuendelea, hivyo tunatoa wito kwa Serikali kuwa makini
katika kushughulikia masuala haya ili yasije yakazua mgogoro mkubwa
zaidi,” alisema mmoja wa waumini wa kanisa hilo.
Hili ni tukio la
pili kubwa kutokea, baada ya lile lilitokea Mbagala ambapo inadaiwa
mtoto wa muumini wa dini ya Kikristu, alikojolea Quaran na kuzua
mtafaruku na vurugu ambazo zilizimwa na jeshi la polisi.
Chanzo - Mtanzania
No comments:
Post a Comment
This is a public viewable website, post something that is not harmful to other people