![]() |
Mhe. John Mnyika mbunge wa Ubungo |
Nikiwa
mmoja wa vijana wa Tanzania na mbunge kijana sikubaliani na utaratibu mzima
ulivyopangwa wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt Fennela
Mukangara kutoa ratiba ya maonyesho na maadhimisho mengine bila kueleza hatua
iliyofikiwa katika utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa vijana katika
maadhimisho kama hayo mwaka 2011 na pia kuweka mkazo katika maonyesho katika
Mkoa mmoja badala ya masuala na matukio muhimu yenye kugusa maisha ya vijana wa
katika maeneo mbalimbali nchini mijini na vijijini.
Ikumbukwe
kwamba Tarehe 4 Oktoba 2012 Waziri alizungumza na vyombo vya habari kueleza
kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Vijana. Waziri alieleza kuwa maadhimisho
hayo yatahusisha maonyesho yatakayoanza tarehe 8 na kufikia kilele chake tarehe
14 Oktoba 2012 kwenye kilele cha mbio za Mwenge na kumbukumbu ya kifo cha
Mwalimu Nyerere mkoani Shinyanga. Waziri ameeleza kuwa mgeni rasmi katika
kilele cha maonyesho na maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.
Hivyo,
natoa mwito kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini kutokubaliana na
utaratibu huo wa kuweka kipaumbele katika maonyesho zaidi badala yake wafanye
maadhimisho kwa kuweka kipaumbele masuala na matukio yenye kugusa maisha ya
vijana na mustakabali wa taifa.
Vijana
tuitumie wiki hiyo kutafakari masuala ya msingi baina yetu ili tuweze kutimiza
wajibu lakini wakati huo huo tuzifuatilie mamlaka zingine zinazohusika na
masuala ya vijana kwa upande wao ikiwemo serikali katika ngazi zote kuhusu
utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa vijana kwa nyakati mbalimbali
katika mwaka 2011.
Kwa
upande wangu, naitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ieleze
hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ahadi kipaumbele kuhusu ajira kwa
vijana na uundwaji wa Baraza la Taifa la Vijana kama ilivyoniahidi bungeni
mwaka 2011 na nyingine kuzirejea bungeni mwaka 2012.
Kuhusu
masuala ya ajira, tulipendekeza bungeni na Wizara ikakubaliana nasi kuanzisha
Benki ya Taifa ya Vijana ili kuwezesha vijana wasioweza kumudu masharti ya
kibenki katika mfumo wa kawaida wa kibenki kuweza kupata mitaji kwa masharti
nafuu kwa ajili ya kujiajiri. Aidha, tulipendekeza na Wizara ikakubali
kushirikiana na Wizara zingine ili kuwe na mfumo wa kuwezesha wahitimu wa vyuo
kutumia vyeti vyao kama dhamana kuweza kukopa katika mabenki kwa ajili ya
kujiajiri.
Kuhusu
uundwaji wa Baraza la Taifa la Maendeleo ya Vijana, serikali iliahidi kwamba
mchakato wa kuundwa kwa baraza hilo ungekamilika katika mwaka wa fedha
2011/2012, hata hivyo mpaka kipindi hicho kinamalizika mwezi Juni 2012 na
kuanza kwa mwaka mwingine wa fedha 2012/2013 ahadi hiyo haijatekelezwa. Baraza
la Taifa la Maendeleo ya Vijana likianzishwa litaweza kuwaunganisha vijana bila
kujali tofauti zao zingine katika kushughulikia vipaumbele mbalimbali vya
vijana ikiwemo katika masuala ya elimu, ajira, afya, michezo na maisha ya
vijana kwa ujumla.
Imetolewa tarehe 5 Oktoba 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Kijana wa Tanzania
No comments:
Post a Comment
This is a public viewable website, post something that is not harmful to other people