Thursday, December 13, 2012

Kawambwa: Waliosoma vyuo vikuu na pesa za mikopo warudishe haraka

 SERIKALI imewataka wote waliokopeshwa kwa ajili ya kusoma elimu ya juu nchini kuirejesha kwa hiari  mikopo hiyo kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) na wasipofanya hivyo watafuatiliwa na wakala maalumu aliyeajiriwa na bodi hiyo kwa ajili ya kuwafuatilia ambao hawajairejesha mpaka sasa.
Imesema mpaka kufika Septemba mwaka huu fedha zilizokusanywa ni Sh23.3 bilioni kutoka kwa watu 48,235 na kwamba kiwango hicho ni chini ya asilimia 50 ya fedha zilizotakiwa kurudishwa, chini ya asilimia 50 ya watu wanaotakiwa kurejesha mikopo hiyo.
Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Televisheni ya ITV, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi , Dk Shukuru Kawambwa alisema suala la urejeshwaji wa mikopo bado ni changamoto kubwa.
“Hawa 48,235 ni wale ambao bodi imewagundua wako wapi na wanafanya kazi gani, wengine hawajagundulika wako wapi  hata hawajitokezi sijui  wanataka mpaka watafutwe,” alisema Kawambwa na kuongeza:
“Bodi imeajiri  wakala maalumu kwa ajili ya kuwafuatilia watu ambao hawajarejesha mikopo, lengo ni kuhakikisha fedha hizi zinakusanywa ili kuwasaidia wanafunzi wengine.
“Nimeiambia bodi kuwa, hatuwezi kuzungumza vizuri kabla ya kufanya kazi nzuri ya kurejesha mikopo, nimewaeleza wazi kwamba hawawezi  kutoa mikopo wakati hawairejeshi ipasavyo, sasa hakuna kulala ni kazi tu,” alisema Kawambwa.
Alifafanua, “Kama waliotakiwa kurejesha mikopo  wangefanya hivyo kwa wakati ni wazi kuwa  idadi ya wanafunzi watakaopata mikopo ingeongezeka kwa kiasi kikubwa, lengo la Serikali ya awamu ya nne ni kuona kila mwanafunzi anapata mkopo.”
Alisema mwaka 2004-2005 wanafunzi 6,000 tu ndiyo waliopewa mikopo na  kwamba mwaka huu idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia wanafunzi 98,000.
Alifafanua Mwaka 2004 -2005 fedha iliyotolewa kwa ajili ya mikopo ni Sh9.9 bilioni na kwamba  bajeti ya mwaka huu ni Sh326 bilioni.
Akizungumzia wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo, Dk Kawambwa alisema kila mwaka taratibu za mikopo zinafanyiwa marekebisho ili ziwe na manufaa zaidi na kwamba hilo limetokana na ushauri mbalimbali kutoka kwa wadau wa elimu nchini.
“Kwanza huwa wanatizamwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao kwa kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuwekeza kwa wanafunzi waliofaulu vizuri zaidi,” alisema Kawamba na kuongeza:
“Lakini baada ya kusikiliza ushauri tulianza kutizama uhitaji zaidi, sasa tunaangalia anayeomba mkopo anahitaji kweli kupewa, pia tunatizama vipaumbele tulivyojiwekea ambavyo ni wanafunzi wanaosomea udaktari, ualimu na uhandisi.”
Alisema kutokana na hali hiyo mwaka huu asilimia 50 ya wanafunzi walioomba mikopo ni walimu.
“Walimu kujiendelea kielimu ni jambo zuri lakini sio kukimbia kufundisha kwa lengo la kusoma, tumewaruhusu baadhi ya walimu kusoma na wengine tutawaruhusu mwakani” alisema Kawambwa.
Akizungumzia suala la wanafunzi kufanyiwa udahili mara mbili, alisema Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) imeanzisha mpango wa awamu ya pili ya kudahili wanafunzi unaoitwa, Mpango wa Pamoja wa Kudahili Wanafunzi (CAS) na kwamba  umetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu.
“Wanafunzi walioomba nafasi  sasa wanaingizwa  katika mfumo huo na kuchambuliwa kulingana na sifa zao hakuna atakayependelewa, kila mwenye sifa atapangiwa fani atatakayosoma” alisema Kawambwa na kuongeza:

No comments:

Post a Comment

This is a public viewable website, post something that is not harmful to other people