
Aliyekuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Marehemu
Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Barlow (52)
--
Mwili wa aliyekuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Marehemu
Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Barlow (52) ambaye alifariki dunia
usiku wa kuamkia Jumamosi kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni
majambazi, utaagwa Jumanne saa tano asubuhi katika kanisa la Katoliki lililoko
Ukonga, jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kamati ya
maandalizi ya mazishi na kuthibitishwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Mrakibu
Msaidizi wa Polisi, Advera Senso, Mwili Marehemu utawasili siku ya Jumatatu
jioni ukitokea mwanza.
Siku ya Jumanne mwili wa marehemu utafikishwa nyumbani
kwake Ukonga kabla ya kupelekwa katika kanisa la Katoliki Ukonga kwa shughuli
za ibada na kutoa heshima za mwisho.
Aliendelea kusema kuwa viongozi mbalimbali wa
Serikali, Maofisa wa waandamizi wa Polisi, Askari na wananchi watatoa heshima
zao za mwisho katika kanisa la hilo.
Aliongeza kuwa baada ya ibada na shughuli ya kuaga
kukamilika, mwili wa marehemu utasafilishwa kuelekea nyumbani kwao kilema,
Moshi vijijini Mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika siku ya Jumatano
mchana kwa taratibu zote za kidini na baadae kuhitimishwa kwa kufuata taratibu
za kijeshi.
Marehemu kamanda Barlow alizaliwa katika kijiji cha
Kyou Wilaya ya Moshi vijijini, Mkoani Kilimanjaro mwaka 1960, baada ya kumaliza
elimu ya msingi mwaka 1974 katika shule ya msingi Lombetha, alijiunga na elimu
ya sekondari katika shule ya Maua Seminary na baadae kujiunga kidato cha tano
na sita katika shule ya Sekondary Milambo na kuhitiku mwaka 1981.
Baaada ya kumaliza elimu ya sekondari, marehemu
kamanda Barlow alilitumikia taifa katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
Operesheni Imarisha katika kikosi cha Mafinga JKT, Mkoani Iringa.
Mwaka 1982, Marehemu alijiunga na Chuo cha mafunzo cha
Polisi Moshi (CCP) kwa ajili ya kusomea mafunzo ya awali ya sheria ya Uhamiaji
na baadae kupangiwa kufanya kazi mpakani mkoani Mtwara akiwa kama Mkuu wa kituo
cha Uhamiaji.
Marehemu kamanda Barlow aliajiriwa na Jeshi la
Polisi baada ya kumaliza shahada ya kwanza ya utawala kutoka Chuo kikuu
cha Dar es Salaam kwa kuomba kazi katika Idara ya Polisi mwaka 1987
katika ngazi ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi.
Kutokana na uadilifu wake katika kazi, Marehemu
aliweza kuaminiwa na viongozi wake na kupandishwa vyeo mbalimbali mpaka kufikia
ngazi ya Cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi, cheo ambacho kilimuwezesha
kupewa madaraka ya kuwa Kamanda wa Polisi Mikoa mbalimbali ikiwemo Tabora na
Mwanza.
Kabla ya kufikia ngazi aliyokuwanayo, marehemu aliwahi
kuaminiwa na kushika nyazifa mbalimbali akiwa kama Mkuu wa Upelelezi Wilaya
(OC-CID), Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na Mkuu Upelelezi Mkoa (RCO) na hatimaye
kupata wadhifa wa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa. Marehemu Kamanda Barlow hadi
umauti unamkuta alikua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na atakumbukwa kwa
juhuda kwa juhudi zake za kupambana na kudhibiti uhalifu.
Na
Tamimu Adam- Jeshi la Polisi
No comments:
Post a Comment
This is a public viewable website, post something that is not harmful to other people